Habari Mpya:MEYA MANISPAA YA DODOMA ATOA RAI KUBORESHA MAONESHO YA WAKULIMA NA WAFUGAJI -bofya hapa kwa habari zaidi.......
Meya
wa Manispaa ya Dodoma Mstahiki Profesa Davis Mwamfupe (wa kwanza kulia)
akishuhudia mmoja ya banda la maonesho alipotembelea Maonesho ya
Nanenane Kanda ya Kati katika Viwanja vya Nzuguni Manispaa ya Dodoma
hivi karibuni.
Na Ramadhani Juma, Dodoma
HALMASHAURI za Manispaa na Wilaya katika mikoa ya Kanda ya Kati
unayoundwa na mikoa ya Dodoma na Singida kwa kushirikiana na wadau
mbalimbali wanaounga mkono shughuli za kilimo, mifugo na uvuvi
wameshauriwa kubuni njia rahisi inayoweza kuwafikishia kwa wakulima na
wafugaji elimu inayopatikana kwenye viwanja vya Maonesho ya Wakulima
maarufu kama Nanenane.
Rai hiyo imetolewa na Meya wa Manispaa ya Dodoma Mstahiki Profesa Davis
Mwamfupe kufuatia maenesho ya Nanenane yaliyomalizika hivi karibuni katika
maeneo mbalimbali nchini, ambapo amesema bado Maonesho hayo hususan
Kanda ya Kati hayajafanikiwa kuwasaidia wakulima, wafugaji na wavuvi wetu
kwa kiasi kinachoridhisha na kuwawezesha kubadili shughuli zao na kuzifanya
kuwa na tija inayoridhisha.
Alisema Maonesho ya Nane Nane yamekuwepo kwa miaka mingi katika Kanda
mbalimbali nchini na yamekuwa na mambo ya kuvutia sana hususani Teknolojia
na mbinu bora za uzalishaji katika kilimo na mifugo ambazo zinauwezo wa kuleta
tija kubwa lakini bado changamoto kubwa ni kwamba mambo yote bora na mazuri
yanayopatikana kwenye Maonesho hayajaweza kumfikia mkulima kwenye ngazi
za msingi kwa maana ya ngazi ya kaya na vijiji.
Alisema kuwa, unaweza kutoka umbali usiozidi kilomita mbili tu kutoka kituo
(Uwanja) cha Maonesho kilipo utashangaa kukuta mkulima analima kilimo cha
kienyeji ambacho hakina manufaa.
“Teknolojia inayooneshwa kwenye Maonesho haya bado haijaweza kuwafikia
wakulima na wafugaji wetu kwenye vijiji vyao wanakoendesha shughuli zao za
kilimo na mifugo” alisema Profesa Mwamfupe na kuongeza kuwa, bado teknolojia
na ubunifu unaopatikana kwenye Maonesho haya unahitaji kuwafikia wakulima wa
chini kabisa.
Alitoa wito kwa Mamlaka zinazohusika kuhakikisha Kiwanja cha Maonesho ya
Nane Nane Kanda ya Kati kilichopo katika Kata ya Nzuguni Manispaa ya Dodoma
kinakuwa kituo cha Shamba Darasa la kilimo mifugo na uvuvi cha kudumu ili
wataalamu wa kilimo na mifugo wawepo kituoni hapo kipindi chote cha mwaka
wakisimamia shughuli za kilimo na mifugo kituoni hapo na Halmashauri zilete
Wakulima na Wafugaji wao kujifunza na kupata suluhisho la changamoto
zinazowakabili katika shughuli zao za uzalishaji.
No comments: